SIASA: JE UNAFAHAMU KUWA JK AMETEUA JUMLA YA MAWAZIRI 120 KWA MUDA WA MIAKA 10 YAKE YA UONGOZI? SOMA HAPA
http://jaridahuru.blogspot.com/2015/02/siasa-je-unafahamu-kuwa-jk-ameteua.html
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ambaye alianza kipindi chake cha kuongoza nchi mwaka 2005 kwa kuteua jumla ya mawaziri na manaibu 60, anaondoka akiwa ameteua jumla ya watu 118 kushika nyadhifa hizo, Mwananchi inaweza kukuthibitishia.
Mwaka 2005 wakati akitangaza baraza lake la kwanza, Rais Kikwete aliteua mawaziri 29 na manaibu 31, idadi ambayo ilikuwa kubwa kulinganisha na marais waliopita, lakini alipofanya mabadiliko ya kwanza makubwa mwaka 2008, alipunguza ukubwa wa Serikali baada ya kuteua mawaziri 26 na manaibu 21.
Hata hivyo, idadi kubwa ya watu walioteuliwa kuwa mawaziri, imechangiwa na idadi ya mabadiliko aliyofanya tangu alipovunja baraza mwaka 2008 kutokana na Edward Lowassa kujiuzulu uwaziri mkuu.
Ukijumlisha na mabadiliko hayo, tayari Rais Kikwete amefanya mabadiliko makubwa ya mawaziri mara tatu na madogo mengine mara tatu, hali inayoifanya Serikali yake kutumia mawaziri tofauti 118 katika utawala wake hadi sasa.
Rais alifanya mabadiliko makubwa ya kwanza mwaka 2008 kutokana na kashfa ya mkataba wa Richmond iliyosababisha Lowassa kujiuzulu na baadaye mwaka 2012 aliwaacha mawaziri sita kutokana na kashfa iliyotokana na ripoti ya CAG, kabla ya kufanya mabadiliko mengine makubwa mapema mwaka 2014 kutokana na kashfa ya Operesheni Tokomeza, ambayo utekelezaji wake ulitawaliwa na uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu.
Katika kipindi hicho, mawaziri wanne walipoteza maisha, mmoja alipata kazi Umoja wa Mataifa na wengine kujiuzulu na hivyo kulazimika kufanya mabadiliko madogo manne.
“Mabadiliko haya ninayachambua katika sehemu mbili. Kwanza, ili mtu aweze kufanya kazi kwa utulivu na kutekeleza mikakati yake ni lazima awe na muda wa kutosha. Kama akikosa utulivu taasisi (wizara) aliyopo inaweza kuyumba,” alisema Mkuu wa Shule ya Sheria wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Profesa Bonaventure Rutinwa.
Hata hivyo, Rutinwa, ambaye alikuwa mmoja wa wasomi waliotakiwa kutoa maoni yao kuhusu idadi ya mawaziri walioteuliwa hadi sasa, alisema mara nyingi mabadiliko hayo yamefanyika kutokana na matatizo yanayotokea katika wizara zilezile, akitoa mfano Wizara ya Nishati na Madini, ambayo alisema imesababisha wizara nyingine kutetereka.
“Ili kuepusha jambo hili. Uteuzi katiza wizara kama hii ya Nishati na Madini unatakiwa kufanywa kwa umakini zaidi ili kuepuka kubadili mawaziri mara kwa mara,” alisema.
“Kama waziri anakuwa na mipango ya muda mrefu na akaondoka ndani ya kipindi kifupi, mambo yanaweza kukwama,” aliongeza.
Kwa upande wa pili, Profesa Rutinwa alisema mabadiliko hayo huondoa fikra kwa baadhi ya mawaziri kuwa uwaziri ni urithi badala ya nafasi hiyo kuwa ya kisiasa.
“Uwaziri utaendelea kuwa wako iwapo tu utafanya vizuri kazi zako. Hata Rais Kikwete wakati akiingia madarakani aliwahi kusema wazi kuwa yeye na Makamu wa Rais ndiyo wenye nafasi za kudumu, si mawaziri aliowateua,” alisema.
Lakini Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Profesa Tolly Mbwete na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana walitofautiana na msomi mwenzao na badala yake kupongeza mabadiliko hayo ya mara kwa mara, wakisema yanaongeza ufanisi.
“Naona ni suala la kawaida tu ili kuondoa ufanyaji kazi wa mazoea,” alisema Profesa Mbwete.
Alisema jambo la muhimu kwa mawaziri ni kufanya kazi ipasavyo na kusisitiza kuwa ndiyo maana mawaziri ambao ni watendaji kazi wazuri wapo mpaka leo.
“Wanaoteuliwa wanatakiwa kutambua wajibu wao, lakini pia waziri kukaa sana katika nafasi hiyo si jambo zuri,” alisema.
Dk Bana alisema: “Mawaziri wanabadilishwa kulingana na uwajibikaji wao. Wapo walioondolewa kwa sababu ya shinikizo au maazimio ya Bunge.”
Alisema kitendo cha Rais Kikwete kubadili Baraza la Mawaziri mara saba kinaonyesha wazi kuwa kiongozi huyo anasikiliza ushauri wa wasaidizi wake na malalamiko yanayotolewa na wananchi juu ya wizara au utendaji wa mtu.
“Mfano mzuri ni mwaka 2006, Rais Kikwete alibadili Baraza la Mawaziri kwa sababu wananchi tulipiga kelele kuwa lilikuwa na mawaziri 60 ambao ni wengi. Amekuwa akibadili ili kuongeza utendaji zaidi,” alisema Dk Bana.
Kwa mujibu wa mapitio ya Mwananchi, Rais Kikwete aliachana na mawaziri 63 kwa sababu tofauti, wakati amedumu na mawaziri 16 tu tangu mwaka 2005 alipoingia Ikulu.
Hivi sasa Baraza la Mawaziri lina mawaziri 55, wakiwamo 16 ambao alianza nao tangu alipotangaza baraza lake la kwanza la mawaziri mwaka 2005.
Waliopo sasa ni Dk Binilith Mahenge, Ummy Mwalimu, Saada Mkuya, Mwigulu Nchemba, Adam Malima, Dk Asha-Rose Migiro, Janet Mbene, Dk Seif Rashid, Dk Stephen Kebwe, Jenista Mhagama, Dk Pindi Chana, Dk Titus Kamani na Kaika Telele.
Wengine ni George Simbachawene, Amos Makala, Godfrey Zambi, Juma Nkamia, Lazaro Nyarandu, Mahmoud Mgimwa, Charles Kitwanga, Charles Mwijage, Anna Kilango- Malecela, Angela Kairuki, Stephen Masele, William Lukuvi na Profesa Makame Mbarawa.
Pia wamo Samwel Sitta, Dk Abdulla Juma Abdulla, Mahadhi Juma Maalim, Pereira Ame Silima, Dk Abdallah Kigoda, Dk Fenella Mukangara, Gerson Lwenge, Dk Charles Tzeba, Dk Harrison Mwakyembe, January Makamba, George Mkuchika na Samia Suluhu Hassan.
Mawaziri ambao Rais Kikwete alianza nao na wapo mpaka sasa ni Sofia Simba, Profesa Mark Mwandosya, Stephen Wasira, Dk Hussein Mwinyi, Dk John Magufuli na Aggrey Mwanry.
Wengine ni Profesa Jumanne Maghembe, Dk Shukuru Kawamba, Hawa Ghasia, Dk Mary Nagu na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye katika Baraza la kwanza, alikuwa naibu waziri na baadaye waziri wa Tamisemi.
Mawaziri wengine alioanza nao mwaka 2005 wakiwa naibu mawaziri ni Gaudencia Kabaka, Bernard Membe, Celina Kombani, Christopher Chiza, Mathias Chikawe na Dk Makongoro Mahanga ambaye tangu 2005 mpaka sasa bado ni naibu waziri.
Mawaziri wengine
Mawaziri waliotemwa au kujiuzulu tangu Rais Kikwete aingie madarakani, wakiwamo wale walioshindwa katika kinyang’anyiro cha ubunge ni Edward Lowassa, Antony Diallo, Dk Ibrahim Msabaha, Basil Mramba, John Chiligati, Andrew Chenge, Joseph Mungai, Dk Emmanuel Nchimbi, Lawrence Masha, Mustafa Mkulo, William Ngeleja, Dk Cyril Chami, Omary Nundu, Bakari Mwapachu na Kingunge Ngoimbale-Mwiru.
Wengine ni Ezekiel Maige, Dk Hadji Mponda, Dk Teresa Huvisa, Shamsi Vuai Nahodha, Nazir Karamagi, Dk Mathayo David, Balozi Khamis Kagasheki, Profesa Anna Tibaijuka, Profesa Sospeter Muhongo, Dk Batilda Buriani, Joseph Mungai, Diodorus Kamala, Mohamed Seif Khatib, Mwantumu Mahiza, Profesa Peter Msola na Profesa David Mwakyusa, Philip Marmo na Dk Juma Ngasongwa.
Manaibu waziri ni Dk Luca Siyame, Balozi Seif Ally Idd, Hezekiah Chibulunje, Shamsa Mwangunga, Daniel Nsanzugwanko, Hezekiah Chibulunje, Rita Mlaki, Dk Charles Mlingwa, Zabein Mhita, Dk Athuman Mfutakamba, Dk Lucy Nkya, Goodluck Ole Medeye, Benedict Ole Nangoro, Gregory Teu, Philipo Mulugo, Mohamed Abood, Dk Aisha Kigoda, Omari Yusuf Mzee, Dk Maua Daftari, Zakia Meghji, Joel Bendera, Abdisalaam Issa Khatib na James Wanyancha, Gaudence Kayombo, Mudhihir Mudhihir.
Mawaziri waliofariki dunia katika kipindi hicho ni Salome Mbatia, Juma Akukweti, Jeremiah Sumari na Dk William Mgimwa.
Mwaka 2006
Katika baraza lake la kwanza Rais Kikwete aliteua mawaziri na naibu mawaziri 60 Januari 2006 na ilipofika Oktoba 2006, Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya kwanza makubwa ya baraza lake la mawaziri kwa kuwahamisha vituo vya kazi mawaziri 10 na naibu mawaziri wanane. Katika mabadiliko hayo hakuna waziri aliyeachwa.
Mwaka 2007
Februari 2007, Rais Kikwete alifanya uteuzi wa mawaziri wawili na manaibu wawili. Alimteua Dk Buriani kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Uratibu) kujaza nafasi iliyoachwa wazi baada ya kifo cha Akukweti. Ngeleja aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini na Kayombo aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwekezaji.
Mwaka 2008
Februari 12, 2008 Rais Kikwete alivunja Baraza la Mawaziri baada ya kujiuzulu kwa Lowassa, Dk Msabaha na Karamagi. Nafasi zao zilizibwa na Ngeleja (Nishati na Madini), Dk Kamala (Afrika Mashariki), huku Pinda akiteuliwa kuchukua nafasi ya Lowassa.
Mei 2008
Baada ya Chenge kujiuzulu Mei, 2008 kutokana na kashfa ya ununuzi wa rada na nafasi yake kujazwa na Mbunge wa Bagamoyo, Dk Kawambwa, Rais Kikwete pia alibadilisha mawaziri kadhaa.
Mwaka 2012
Rais Kikwete alifanya mabadiliko Mei 2012 kwa kuwaondoa Mkulo (Fedha), Ngeleja (Nishati na Madini), Dk Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Maige (Maliasili na Utalii), Nundu (Uchukuzi) na Dk Chami (Viwanda na Biashara). Dk Mfutakamba (Naibu, Uchukuzi) na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Nkya.
Badala yao aliwateua Dk Mgimwa (Fedha), Balozi Kagasheki (Utalii), Dk Mwakyembe (Uchukuzi), Dk Kigoda (Viwanda na Biashara), Dk Mwinyi (Afya), Profesa Muhongo (Nishati na Madini), Dk Seif Rashid (Naibu, Afya) na George Simbachawene (Naibu, Nishati na Madini).
Manaibu wapya walioingia ni Makamba (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia), Dk Tzeba (Uchukuzi) na Makala (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo). Wengine ni Dk Mahenge (Maji), Masele (Nishati na Madini), Kairuki (Katiba na Sheria), Mbene na Mkuya (Fedha).
Januari 2014
Rais Kikwete alifanya mabadiliko mengine Januari 19, 2014 kwa kuteua mawaziri wapya wawili na naibu mawaziri wapya wanane, huku akiwapandisha vyeo manaibu mawaziri wanne kuwa mawaziri kamili.
Aliwapumzisha Dk Huvisa, Teu, Mulugo, Ole-Nangoro na Ole-Medeye.
Mabadiliko hayo yalikuwa yanalenga kujaza nafasi zilizoachwa na Balozi Kagasheki, Dk Nchimbi, Nahodha na Dk Mathayo waliotemwa Desemba 2013 kutokana na kashfa ya Operesheni Tokomeza na nafasi ya Dk Mgimwa, aliyefariki dunia kutokana na maradhi.
Mawaziri wapya walioteuliwa wakati huo ni Dk Migiro, Dk Kamani, Nchemba, Dk Kebwe, Mhagama, Dk Chana, Telele, Zambi, Nkamia na Mgimwa.
Waliopandishwa kuwa mawaziri ni Mkuya, Nyalandu, Dk Rashidi, Dk Mahenge na Dk Mwinyi aliyehamishwa kutoka Afya na Ustawi wa Jamii kwenda Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na wengine kadhaa walihamishwa.
Januari 2015
Rais alifanya mabadiliko yake yanayoweza kuwa ya mwisho Januari 2015, akijaza nafasi zilizoachwa wazi na mawaziri wawili, Profesa Tibaijuka (kufutwa kazi) na Profesa Muhongo kujiuzulu kutokana na kuhusishwa na kashfa ya Tegeta Escrow.
Walioingia ni manaibu waziri wawili, Mwijage (Nishati na Madini) na Kilango- Malecela (Elimu na Mafunzo ya Ufundi), huku wengine wakihamishwa.