KITAIFA: WAFUASI WA SHEHEPONDA WAFUNGA BARABARA MJINI MOROGORO NA KUSWALI CHINI YA ULINZI MKALI
http://jaridahuru.blogspot.com/2015/02/kitaifa-wafuasi-wa-sheheponda-wafunga.html
SHEHE Ponda balaa! hali ni tete kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro ambayo inasikiliza kesi ya Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam, Shehe Ponda Issa Ponda anayekabiliwa na shitaka la kutoa maneno ya uchochezi, Amani lina mtiririko wa habari.
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam, Shehe Ponda Issa Ponda.
Juzi, wakati kesi ikiendelea kusikilizwa mahakamani hapo, baadhi ya wafuasi wa Shehe Ponda waliokuwa wamefika kusikiliza kinachoendelesa, waliamua kutoka nje na kufunga barabara ili kuswali swala ya adhuhuri (saa 7 mchana).
WAFUNGA BARABARA KWA BAISKELI
Huku wakionekana kuwa waumini wazuri wa imani yao, wafuasi hao walifunga barabara kwa kutumia baiskeli na kufanya ibada ya hatua kwa hatua.
WATOA SAUTI KAMA KAWAIDA
Katika ibada hiyo, wafuasi hao walikuwa wakitoa sauti za juu kama inavyokuwa wanapokuwa kwenye nyumba rasmi ya ibada hali iliyoashiria kuwa, walikuwa kiroho zaidi.
WAMFUATISHA IMAMU
Ili kuonesha kuwa taratibu yote ya ibada inafuatwa, mfuasi mmoja aliyesemekana ni imamu alikuwa akiwaongoza wafuasi hao katika kila hatua. Alikuwa akisema Allahu Akbar (Mungu mkubwa) na waumini waliitikia moyoni kisha kufanya alivyokuwa akifanya imamu huyo kama vile kupiga magoti na kusujudu.
Wafuasi wa shehe Ponda wakisali.
POLISI HAWANA NENO
Baadhi ya wafuasi hao walionekana kuwahofia askari polisi waliokuwa wakilinda amani kwenye mahakama hiyo lakini polisi hao walionesha kutokuwa na neno wala dalili ya kukwazwa na wafuasi hao kuswali barabarani.
“Sisi kama polisi hatuna shida, wao ni waumini, muda wa kuswali umefika na hakuna nyumba ya ibada, sasa kwa nini tuwabughudhi.“Isitoshe watu wenyewe wanaonekana watulivu japokuwa awali baadhi yao walidhani sisi tutawavamia lakini waendelee tu, tuko pamoja nao,” alisema afande mmoja alipozungumza na Amani wakati swala hiyo ikiendelea nje ya mahakama.
MFUASI AZUNGUMZA
Baada ya swala hiyo iliyoonekana kuwa na imamu, Amani lilibahatika kuzungumza na mfuasi mmoja ili kujua imani yao inasemaje kuhusu muumini kuswali eneo kama lile.“Si kosa kwa imani yetu.
Shehe Ponda akishuka kwenye gari huku kukiwa na ulinzi mkali.
Dini inaruhusu endapo muumini au waumini watakutwa na kipindi cha swala wakiwa katika eneo ambalo halina nyumba ya ibada basi wanaweza kuswali popote pale ilimradi mbele yao waweke uzio wa kitu,” alisema mfuasi mmoja akijitaja kwa jina la Mohammed.
Swali: “Sasa pale kama wangetokea watu wabaya na kutibua ibada yenu mngeendelea na swala mpaka mwisho au?”Mfuasi: “Hilo lingekuwa tatizo jingine. Huenda maamuzi yangepatikana palepale kutokana na hekima ya wakati huo.”Swali: “Kwa nini msingeenda kwenye nyumba ya ibada kwa kutoka mapema hapa mahakamani?”Mfuasi: “Ilikuwa lazima tuwepo jirani ili tujue kesi inavyoendelea.”
MKE WA PONDA
Miongoni mwa watu wanaohudhuria kesi hiyo ambayo sasa inasikilizwa mfululizo ni mke wa Shehe Ponda, Khadija Ahamad ambaye kila siku anatokea mahakamani hapo mpaka kesi inapoahirishwa.
Alipopatikana na Amani kumtaka aseme lolote kuhusu mumewe na hali ya kesi, alisema hana la kusema kwa sasa wala baadaye.
WATUMISHI WA MAHAKAMA WANAVYOSEMA
Baadhi ya watumishi wa mahakama hiyo waliozungumza na Amani walisema ni mara yao ya kwanza kuona kesi ikiendeshwa kuanzia asubuhi hadi saa tisa alasiri.“Hii ni mpya, Shehe Ponda kaweka utaratibu mgeni kwetu. Hatujawahi kuona kesi ya mtu inaanza asubuhi hadi saa tisa alasiri, muda wa kazi wa serikali unapomalizika,” alisema mtumishi mmoja bila kutaja jina lake.
Kuhusu muda wa kesi mpaka hukumu, mtumishi huyo alisema kutokana na mashahidi kuwa wengi anakadiria kesi hiyo inaweza kuchukua siku kumi na nne.“Mh! Mashahidi ni wengi sana, huenda ikaenda mpaka siku kumi na nne ndipo hukumu itatolewa. Ni shida kwa kweli,” alisema mtumishi huyo.
KUMBUKUMBU ZA NYUMA
Shehe Ponda alikutwa na madai hayo Agosti 10, mwaka 2013 mjini Morogoro. Kwa maana hiyo, amekuwa mahabusu tangu mwezi huo mpaka sasa ambapo ni kama siku 547.