SIASA: MBOWE AKOMESHWA NA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA, AMPIGA 'STOP' KUGOMBEA TENA UENYEKITI CHADEMA
http://jaridahuru.blogspot.com/2014/07/siasa-mbowe-akomeshwa-na-msajili-wa.html
Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imesema haitambui kuondolewa kwa kipengele cha ukomo wa uongozi uliofanywa na Chadema bila kufuata idhini ya mkutano mkuu wa chama hicho.
Mwaka 2006, Katiba ya Chadema ilifanya marekebisho
yaliyoruhusu wanachama kugombea uongozi bila ukomo wakati awali,
waliruhusiwa kugombea kwa vipindi viwili vya miaka mitano.
Barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis
Mutungi kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chadema, inasema kipengele hicho
katika Ibara ya 6.3.2 (C) kiliondolewa kwenye katiba bila idhini na
mkutano mkuu wa chama hicho. Mutungi alisema baada ya kupitia muhtasari
wa kikao cha mkutano mkuu wa mwaka 2006 suala la kuondoa kipengele cha
ukomo wa uongozi halikuonyesha kujadiliwa katika mkutano huo.
Hata hivyo, akizungumza kwa simu jana, Katibu Mkuu
wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema kipengele hicho kiliondolewa kwa
vikao vya chama ambavyo ni wilaya na mkoa.
“Mjadala kuhusu ukomo wa uongozi ulishamalizika na
haujadiliwi tena, ulishapitishwa na vikao halali vya chama, mkutano
mkuu ulipitisha yale yaliyoamuliwa na vikao vya chini,” alisema Dk Slaa.
Hata hivyo, Jaji Mutungi alisema: “Chadema wamefanya mabadiliko bila kufuata katiba”
Alishauri waitishe mkutano rasmi na halali kwa mujibu wa katiba ya chama hicho ili waweze kurekebisha kasoro zilizopo.
Alisema kama chama hicho hakitarekebisha kasoro hiyo, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa haiwezi kuitambua ibara hiyo.
Alisema ingawa hoja hiyo iliwasilishwa na
aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba ambaye
sasa si mwanachama wake, bado hoja hiyo ni muhimu na inahitaji kufanyiwa
kazi.
“Ni vizuri mkaifanyia kazi hoja hiyo bila kujali
kwamba aliyeiwasilisha si mwanachama tena wa Chadema,” alisema katika
barua hiyo