MICHEZO: MANJI ACHOMOZA TENA NA LINGINE
http://jaridahuru.blogspot.com/2014/05/michezo-manji-achomoza-tena-na-lingine.html
BAADA ya kimya cha muda mrefu, Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Yusuf Manji ameibuka na kuzungumzia mambo kadhaa ya klabu hiyo, akibariki kuondoka kwa wachezaji wawili nyota, Didier Kavumbagu na Frank Domayo, na kutamba kuwa timu hiyo itasajili wazuri zaidi ya hao.
Amesema kuondoka kwa Kavumbagu na Domayo si mwisho wa timu yao, kwani uongozi wake unaendelea na mipango ya kuhakikisha inasajili wengine wazuri kulingana na mahitaji ya benchi la ufundi.
Aidha, amelifuta Tawi la Tandale jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa mipango ya kujenga uwanja wa kisasa wa klabu hiyo iko pale pale, lakini hawatajenga nje ya jiji hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya klabu, Jangwani jana, Manji alisema kuondoka kwa Kavumbagu ni kutokana na kuchelewa kwa majibu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), juu ya idadi ya wachezaji wageni kwa msimu mpya, huku Domayo ambaye tangu mwaka jana aliombwa kuongeza mkataba, alikuwa akitoa sababu ya kumsubiri mjomba wake ndipo afanye hivyo.
Manji alisema licha ya kuondoka kwa wachezaji hao, bado kwa kushirikiana na aliyekuwa Kocha Mkuu, Hans van de Pluijm, watahakikisha Yanga inafanya vizuri msimu ujao kwenye mashindano ya kimataifa.
Alisema kwamba usajili utafanyika baada ya uchaguzi ili kuepukana na lawama kwa uongozi mpya kuwa ameleta wachezaji wabovu.
“Watu wasione kuwa uongozi uliopo umezembea kwani tulikuwa tunaisubiri TFF, lakini pia, tutambue kuwa wachezaji hao si kwamba wana kiwango kikubwa kama cha wachezaji wa kimataifa Lionel Messi au Cristiano Ronaldo isipokuwa hata tukiwatafuta Kariakoo tutawapata,” alisema Manji.
Alifafanua kuwa Mrisho Ngassa alikwenda Azam FC akarudi, hivyo hata Domayo atarudi Yanga, huku akieleza kuwa mshambuliaji mtukutu wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi, ana mkataba wa miaka miwili na nusu kucheza Jangwani.
Domayo na Kavumbagu ambao walitoa mchango mkubwa kuiwezesha Yanga kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu msimu uliomalizika, wamekimbilia kwa mabingwa wapya wa Tanzania Bara, Azam FC ambako wamesaini mkataba wa miaka miwili na mwingine wa mwaka mmoja.
Katika hatua nyingine, Manji ambaye ni mfanyabiashara tajiri nchini, alitangaza kulifuta rasmi Tawi la Tandale kutokana na kuwa chanzo cha vurugu na migogoro ndani ya klabu.
Pia amewafuta uanachama wanachama sita kwa kukiuka Katiba ya Yanga kwa kwenda kuzungumza na vyombo vya habari bila idhini ya uongozi, huku wakishindwa kulipia ada zao kwa zaidi ya miezi sita.
Hao ni Ally Kamtande, Isiaka Dude, Hamisi Matandula, Waziri Jitu Ramadhani, Mohamed Kigali Ndimba na Selaman Hassan Migali.
Kuhusu suala la kuombwa na wanachama kugombea nafasi hiyo kwa mara nyingine, alisema atalizungumzia siku ya mkutano wa mabadiliko ya Katiba utakaofanyika Juni mosi mwaka huu katika Ukumbi wa Bwalo la Polisi Oysterbay na kuomba wanachama wote kulipia ada zao ili kuhudhuria.
Kuhusu ujenzi wa uwanja wa kisasa eneo la Jangwani, alisema bado nia ipo pale pale, na kwamba kwa vile sio bahari watajenga katikati ya mji kwani wao ni “watoto wa mjini.”
Pia, alisema kikubwa kinachosubirwa ni majibu ya Serikali juu ya maombi ya eneo la ziada, kwani Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alisema suala hilo lipo ukingoni na muda si mrefu watapewa jibu.
Alipoulizwa anachojivunia katika uongozi wake, alisema hakuna jambo la muhimu aliloifanyia Yanga ili ajivunie.
Chanzo: Habari leo