JAMII: MAMA MARIA NYERERE ALIA NA WANAOLICHAFUA JINA LA MUASISI WA TAIFA LA TANZANIA
http://jaridahuru.blogspot.com/2014/05/jamii-mama-maria-nyerere-alia-na.html
Mama Maria Nyerere amezungumza na vyombo vya habari nyumbani
kwake Msasani, na kuwataka vijana waliokwenda kumtembelea kuzunguka nchi
mzima kuwaambia ukweli watanzania juu ya Maisha halisi ya mwalimu na
mchango wake katika ujenzi wa Taifa huru la Tanzania.
Vijana wazalendo na wapenda Amani
ambao wamemtembea Mama Maria wakiongozwa na Kiongozi wao anayejulikana
kwa Jina la Mohamed Nyundo, wamesema wako pamoja na familia hiyo na
kwamba wamesikitishwa na kampeni inayoendelea ya kumchafua Baba wa
Taifa, kumkebehi na kumtuhumu kwa Uzushi na uzandiki.
UJUMBE WA VIJANA KULAANI VITENDO VIOVU VYA KUMVUNJIA HESHIMA BABA WA TAIFA.
Kumekuwepo na kampeni yenye nia
ovu iliyoasisiwa hivi karibuni ya kuharibu taswira na heshima ya Baba wa
Taifa Mwalimu Kambarage Nyerere katika jamii ya kitanzania na
kimataifa. Kampeni hiyo inayoendeshwa na vibaraka wa nchi za magharibi
na Ulaya, wazandiki na maadui wa Amani ya Tanzania imeendelea kusambazwa
kwa kasi na kwa gharama kubwa.
Kutokana na kuwepo kwa Kampeni
hiyo, jumuiko la Vijana Wazalendo na wapenda Amani tumeamua kutoa tamko
hili la kulaani na kupinga vitendo viovu vya baadhi ya watu kumtuhumu,
kumkebehi na kumtukana Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Kwa kutambua Mchango wa Baba wa
Taifa kama muasisi wa Taifa hili, mpigania Uhuru shupavu, Shujaa
aliyekuwa na mapenzi ya dhati kwa watu wake na kwa kutambua umahiri na
jitihada za kujenga Taifa lenye Muungano, Umoja, Amani na Utulivu,
jumuiko la Vijana wazalendo limeamua kuukumbusha Umma wa watanzania juu
ya mchango wa utumishi uliotukuka wa Mwalimu Nyerere katika ustawi wa
Taifa letu, lakini pia kuhamasisha watanzania hasa Vijana kuenzi kwa
Vitendo moyo wa kujituma,weledi na busara za kiuongozi, pamoja na
ushujaa na ushupavu wa Mwalimu Nyerere.
Sisi Jumuiko la Vijana wazalendo,
tumeona ni vyema kuja kumfariji Mama yetu, Mama Maria Nyerere pamoja na
familia nzima ya Mwalimu Nyerere na Kwamba sisi kama wananchi na Vijana
makini tutaendelea kuwa pamoja na familia katika kupinga na kulaani
vitendo hivyo viovu vya kejeli, matusi, tuhuma na kebehi zinazoelekezwa
kwa Baba wa Taifa, marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Kwa masikitiko makubwa,
tumeshitushwa na kufadhaika kuona chombo kikubwa na taasisi muhimu
ambayo ni muhimili mkubwa wa Serikali kama Bunge la Jamhuri la Muungano
wa Tanzania linakuwa ndio uwanja wa matusi ya kumtukana muasisi wa Taifa
hili, imetusikitisha na kutufedhehesha. Imefika wakati sasa, kwa
Bunge Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kudhibiti na kuondoa
kinga yake kwa wale wote ambao kwa ujinga na kutumika wameamua kuanzisha
na kuendesha kampeni kabambe ya kutia doa taswira na heshima ya Baba wa
Taifa.
Chanzo:Fullshangwe