BUNGENI: MKURUGENZI WA UDA KIKAANGONI BUNGENI, ATAKIWA KUTOA MAELEZO KWA KUINGILIA UHURU WA BUNGE
http://jaridahuru.blogspot.com/2014/05/bungeni-mkurugenzi-wa-uda-kikaangoni.html
Mkurugenzi mtendaji wa UDA Robert Kisena katika hafla ya kukabidhiwa mabasi ya UDA |
Dodoma. Mgogoro wa uwekezaji katika Shirika la
Usafirishaji Dar es Salama (Uda) umechukua sura mpya baada ya Bunge
kuamua Mkurugenzi wa Simon Group inayoendesha shirika hilo, Robert
Kisena ahojiwe na Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge kutokana na
kuingilia kati madaraka hayo.
Agizo hilo lilitolewa na Spika wa Bunge, Anne
Makinda alipokuwa akijibu hoja iliyotolewa na Mbunge wa Ubungo
(Chadema), John Mnyika ambaye alitaka tuhuma zilizotolewa na Kisena
dhidi ya Bunge na wabunge zijadiliwe kwa sababu ameingilia uhuru na
kinga za Bunge kwa kuzungumza nje ya Bunge masuala ambayo yametolewa
maelezo na Serikali bungeni.
Hoja ya Mnyika ilitokana na taarifa za baadhi ya
magazeti yaliyotolewa Mei 19, mwaka huu yakimnukuu Kisena akisema kuwa
wabunge wa Dar es Salaam wamehongwa na mfanyabiashara mmoja na kwamba
kampuni yake inamiliki hisa nyingi tofauti na majibu ya Serikali
bungeni.
Akinukuu majibu ya Serikali katika swali
lililoulizwa na Mbunge wa Kawe (Chadema) Halima Mdee, Mnyika alisema
kuwa Serikali ililieleza Bunge kuwa mgawanyo halali wa hisa za Uda upo
kama ulivyosajiliwa kwa msajili wa mashirika ya umma, kwamba shirika
hilo linamilikiwa na Serikali na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Katika kujenga hoja yake Mnyika alisema majibu
hayo yalionyesha kuwa Uda ni Shirika la Umma, jambo ambalo lilipingwa na
Kisena kupitia mkutano wake na waandishi wa habari, akisema Uda
inamilikiwa na kampuni yake kwa asilimia 76.
Alisema kuwa mwekezaji huyo ameingilia haki, kinga
na madaraka ya Bunge kinyume na utaratibu na kuanza kuwatuhumu wabunge
ambao walisema ukweli ndani ya Bunge.
Mnyika alisema uhuru wa Bunge wa mawazo umehojiwa
nje ya Bunge kinyume cha kanuni, kinga na haki za Bunge jambo ambalo ni
hatari kwa mustakabali wa Bunge.
“Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja na wabunge
wenzangu naomba waniunge mkono ili jambo hili liweze kujadiliwa ili
Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge imuite na ahojiwe
kikamilifu,” alisema Mnyika.
Baada ya hoja hiyo, wabunge wengi walisimama kwa
pande zote bila ya kujali itikadi zao za vyama wakiongozwa na wabunge wa
Mkoa wa Dar es Salaam.
Hata hivyo, Spika Makinda alisimama na kuwataka
waketi, ndipo akatangaza kuwa suala hilo haliwezi kujadiliwa bungeni,
bali kamati husika itamuita Kisena na kumhoji.
Kisena hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo na
hata alipopigiwa, simu yake iliita bila ya kupokewa na alipotumiwa
ujumbe wa maandishi hakujibu.