BUNGENI: MISHAHARA YA WAFANYAKAZI VIJIJINI KUTUMWA KWA NJIA YA SIMU
http://jaridahuru.blogspot.com/2014/05/bungeni-mishahara-ya-wafanyakazi.html
Amesema watumishi wengi wa maeneo ya pembezoni mwa nchi (vijijini) hucheleweshewa mishahara yao na kulazimika kuifuata mbali na vituo vyao vya kazi.
“Je, ni kwa nini Serikali isitumie njia za kutuma fedha kwa njia ya simu za mkononi kama vile M-Pesa na Tigo-Pesa ili kuwasaidia watumishi wa vijijini kupata mishahara yao kwa wakati,” aliuliza mbunge huyo.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alisema Serikali inatambua umuhimu wa huduma ya M-Pesa na Tigo-Pesa katika kutoa huduma za kifedha kwa wananchi kwa kutumia mtandao wa simu za mkononi.
“Vile vile Serikali inatambua kuwa huduma hizo kwa sasa imeunganishwa na mabenki yanayotoa huduma hapa nchini, mojawapo ya benki hizo ni pamoja na National Microfinance Bank, CRDB, Benki ya Posta na nyingine,” alisema Nchemba.
Alisema kwa wakati huo huo, Serikali kupitia Wizara ya Fedha huwalipa watumishi wote wa umma mishahara yao kupitia akaunti za watumishi zilizopo kwenye mabenki mbalimbali.
“Kwa kuwa malipo ya walimu yanapitia katika mabenki na kwa kuwa huduma za M-Pesa na Tigo-Pesa kwa sasa zimeunganishwa na mabenki, Serikali inashauri kuwa walimu wajisajili na huduma za kimtandao za mabenki wanakopitishia mishahara yao ili na wao waweze kutumia huduma hizo muhimu,” alisema Naibu Waziri wa Fedha.
Wakati huo huo, serikali imesema kwa sasa inaandaa mkakati wa kitaifa wa elimu ya kifedha nchini, wenye lengo la kumlinda mtumiaji wa fedha.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Devota Likokola (CCM).
Katika swali lake, Likokola alitaka kufahamu Serikali ina wajibu gani katika kuhamasisha, kuwekeza na kuanzisha benki za jamii, wajibu huo unatekelezwa na wilaya ngapi nchini na lini itakamilisha uhamasishaji wa uwekezaji katika benki za kijamii.
Nchemba alisema katika kumlinda mtumiaji wa huduma za kifedha, Serikali itamuelimisha haki na wajibu wake katika zoezi zima la upokeaji na utumiaji wa huduma hizo.