BUNGENI: ELIMU YA TANZANIA USANII MTUPU,KUGUSHI VYETI KWAONGEZEKA, JK AOMBWA KUUNDA TUME
http://jaridahuru.blogspot.com/2014/05/bungeni-bajeti-ya-elimu-kizungumkuti.html
Dodoma/Dar. Baadhi ya wabunge jana
walichachamaa wakisema elimu nchini ipo mahututi na kumtaka Rais Jakaya
Kikwete kuunda tume ya kudumu ya elimu itakayochunguza mfumo wa elimu
nchini.
Wabunge hao walikuwa wakichangia hotuba ya
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
kwa mwaka wa fedha 2014/2015 iliyowasilishwa na waziri wake, Dk Shukuru
Kawambwa Jumamosi usiku.
Wabunge walichachamaa na kudai baadhi ya wabunge wanaelimu za kubabaisha na vyeti vya kufoji.
Wabunge walichachamaa na kudai baadhi ya wabunge wanaelimu za kubabaisha na vyeti vya kufoji.
Mbunge wa Longido (CCM), Lekule Laizer
alipendekeza safari zote za wabunge na mawaziri nje ya nchi zifutwe na
fedha zake zipelekwe kuboresha shule za kata.
Mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia
alizungumzia uduni wa vitabu na mitihani ya wanafunzi wa shule za msingi
akisema inakosewa kutungwa.
“Nina mtihani wa majaribio wa darasa la saba ambao
haufanyiki. Niliwahi kumpa profesa mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM) ambaye alitumia saa mbili na nusu bila kupata jibu lolote
la kuandika. Mtihani wenyewe haufanyiki,” alisema Mbatia na kutoa ofa ya
Sh10 milioni kwa profesa mwingine yeyote bungeni ambaye ataweza kufanya
mtihani huo na kupata alama 100.
“Haya ni madudu ya kutisha. Mwaka jana nilivyotoa
maoni yangu hapa na waziri akasema maoni yetu yamechukuliwa, alisema
rasimu ya mwisho sera ya elimu imepelekwa Baraza la Mawaziri Machi 2013,
lakini hadi sasa bado haijakamilika,” alisema na kuongeza kuwa hiyo ni
dalili ya Bunge kutoheshimiwa.
Pia alizungumzia ripoti za kamati zilizoundwa
kuchunguza elimu lakini hazikufanyiwa kazi na badala yake zikawekwa
kwenye makabati.
“Tumwombe Rais aunde Tume ya Kudumu ya Elimu kwa
sababu kwa hali inavyokwenda ni mbaya sana na napendekeza tume hii
ishughulike na kudhibiti mambo yote yanayofanya kutetereka kwa ubora
elimu nchini.
Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba
alisema elimu ya Tanzania iko mahututi na kuwaomba wabunge kuacha siasa
katika elimu.
“Bajeti itapita lakini tunaua kizazi kijacho.
Mheshimiwa mwenyekiti nenda darasa la kwanza mpaka la saba anayoyasema
Mbatia yapo hata kama hatuyapendi lazima tuseme ukweli,” alisema.
Alisema ukienda katika vyuo vikuu ni majanga.
“Kama unajiangalia wewe na familia yako, basi tunaliua Taifa. Nimefanya
utafiti kwenye nchi 35, Tanzania ni nchi ya mwisho kwa ufaulu,” alisema
na kuongeza kuwa nchi zote zilizoendelea kiuchumi, kiwango cha ufaulu ni
juu ya asilimia 60.
Mbunge wa Ngara (CCM), Deogratias Ntukamazina alisema hakuna Wizara ya Elimu baada ya elimu ya sekondari na msingi kuondolewa.
“Mbele ya Waziri Mkuu niseme kuwa sasa hatuna Wizara ya Elimu…
na sasa wanaondoa elimu ya watu wazima, shule zote za mazoezi
zimeondolewa.”
Mbunge wa viti maalumu (CUF), Magdalena Sakaya
alisema anashangazwa na wizara kushusha madaraja ya ufaulu ambayo awali,
kuanzia alama 34 ilikuwa ni daraja O lakini leo ni ufaulu.
“Kiukweli waziri aliyeko katika wizara hii
ameshindwa kusaidia elimu nchini. Tangu ameshika wadhifa huo anazidi
kubebwa. Kwa nini tunambeba mtu ambaye ameshindwa kusaidia elimu
nchini?” alihoji.
Safari za nje
Laizer alitaka safari za mawaziri na wabunge nje
ya nchi zifutwe na fedha hizo ziboreshe shule za kata ambako ndiko
watoto wa maskini wanakosoma.
Alisema anashindwa kuunga mkono bajeti ya wizara
hiyo wakati watoto wake wote katika jimbo lake wanafeli kutokana na
shule za kata kutokuwa na walimu wa kutosha.
Akifanya majumuisho, Waziri Kawambwa alikiri deni la Sh61 bilioni la madai ya walimu, lakini akasema serikali imekuwa ikilipa.
Alisema kuanzia Agosti mwaka jana hadi Machi,
jumla ya Sh16 bilioni zimelipwa na kwamba si kweli kwamba deni hilo
limebakia kuwa Sh61 bilioni.
Imeandikwa na Sharon Sauwa, Daniel Mjema (Dodoma) na Julius Mathias (Dar).
Chanzo:Mwananchi