MEI MOSI : Je unajua maana ya Mei Mosi?
http://jaridahuru.blogspot.com/2014/04/mei-mosi-je-unajua-jua-maana-ya-mei-mosi.html
Wewe hufikiria nini unaposikia Mei Mosi? Magwaride na maandamano? Kucheza dansi kuzunguka nguzo ya Mei? Au, siku ya mapumziko?
IKITEGEMEA
unakoishi, watu huwa na maoni tofauti-tofauti kuhusu Mei Mosi. Hata
hivyo, maoni hayo yanatokana na chanzo kimoja. Kuchunguza kifupi chanzo
cha Mei Mosi kutatusaidia kuelewa maana ya siku hiyo leo.
Asili ya Mei Mosi
Katika Roma ya kale, siku ya
kwanza ya Mei ilikuwa sikukuu ya Floralia, iliyopewa jina la Flora,
mungu wa majira ya masika na wa maua. Ulikuwa wakati wa kuimba, kucheza
dansi, na magwaride yaliyopambwa kwa maua. Makahaba wa Roma hasa
waliifurahia sikukuu hiyo, kwa kuwa walimwona Flora kuwa mungu wao mkuu.
Waroma walipoanza kumiliki nchi
nyingine, walisambaza desturi zao huko. Hata hivyo, katika nchi za
Kiselti, Waroma walitambua kwamba tayari siku ya kwanza ya Mei ilikuwa
ikiadhimishwa ikiwa sikukuu ya Beltane. Jioni iliyotangulia sikukuu
hiyo, mwanzo wa siku ya Kiselti, mioto yote ilizimwa, na jua
lilipochomoza, watu waliwasha mioto mikubwa kwenye vilele vya vilima au
chini ya miti mitakatifu ili kukaribisha majira ya kiangazi na mwanzo
mpya wa uhai. Ng’ombe walipelekwa malishoni, nayo miungu iliombwa ilinde
ng’ombe hao. Muda si muda, Floralia na Beltane ziliungana na kuwa
sikukuu ya Mei Mosi.
Huko Ujerumani na katika nchi za
Skandinavia, sikukuu hiyo iliitwa Walpurga. Sherehe zilianza Usiku wa
Walpurga kwa kuwasha mioto mikubwa ili kufukuza wachawi na pepo. Katika
nchi nyingine za Ulaya, Mei Mosi iliadhimishwa kwa njia tofauti-tofauti,
na baadhi ya njia hizo zingalipo.
Makanisa ya Kikristo hayakuwa na uvutano mkubwa katika sikukuu hizo za kipagani. Gazeti moja la Uingereza (Guardian)
linasema: “Katika kalenda, Mei Mosi—au Beltane—ndiyo iliyokuwa siku
ambayo kila mtu angefanya apendavyo, sikukuu pekee ambayo kanisa
la Kikristo au mamlaka nyingine yoyote haingeweza kudhibiti.”
Desturi za Mei Mosi
Kufikia Enzi za Kati, desturi
mpya zilikuwa zimeongezwa katika sikukuu hiyo iliyopendwa sana huko
Uingereza. Wanaume kwa wanawake walikesha vichakani wakikusanya maua na
matumba ili ‘kuukaribisha mwezi wa Mei’ jua likichomoza.* Kulingana na trakti moja ya Philip Stubbes (The Anatomy of Abuses),
uasherati ulikuwa umeenea sana. Wapenda-anasa walisimamisha Nguzo ya
Mei katikati ya kijiji, ambapo watu walicheza dansi na michezo mingine
wakiizunguka nguzo hiyo mchana kutwa. Stubbes aliiita nguzo hiyo “Sanamu
yenye kuchukiza.” Watu walimteua malkia wa Mei, na mara nyingi pia
walimteua mfalme wa Mei, ili kusimamia sherehe hizo. Katika sehemu
mbalimbali za Ulaya pia, kulikuwa na Nguzo za Mei na malkia wa Mei.
Desturi zote hizo za Mei Mosi zilikuwa na umuhimu gani? Kichapo kimoja (Encyclopædia Britannica)
kinaeleza hivi: “Mwanzoni sherehe hizo zilikusudiwa kuhakikisha kwamba
kungekuwa na mazao mengi, na pia ng’ombe na watu wangezaana kwa wingi,
lakini katika visa vingi kusudi hilo la awali lilipotea pole kwa pole,
na mazoea hayo yakaendelezwa katika sherehe zinazopendwa na wengi.”
Mapendezi Mbalimbali
Wanaharakati wa Uprotestanti
walijaribu kuondolea mbali sikukuu hiyo iliyoonwa kuwa ya kipagani.
Scotland iliyokuwa imeathiriwa na mafundisho ya Calvin ilipiga marufuku
sikukuu ya Mei Mosi katika mwaka wa 1555. Kisha Bunge la Uingereza
lililokuwa likiongozwa na Waprotestanti likapiga marufuku Nguzo za Mei
katika mwaka wa 1644. Katika kile kipindi cha Jumuiya ya Madola, wakati
ambapo hakukuwa na mfalme huko Uingereza, “mazoea mapotovu” ya Mei Mosi
yalipigwa marufuku. Hata hivyo, katika mwaka wa 1660, kulipokuwa na
mfalme tena, Nguzo za Mei zilianza kutumiwa tena.
Sherehe za Nguzo ya Mei
zilipungua hatua kwa hatua katika karne ya 18 na mwanzoni mwa karne
ya 19 lakini zimeanza kuongezeka tena hivi karibuni pasipo upotovu
uliokuwapo awali. Desturi nyingi za Mei Mosi, kama vile watoto kucheza
dansi wakizunguka Nguzo ya Mei wakisokota tepe zenye rangi mbalimbali,
zimeanza majuzi. Hata hivyo, watafiti wa desturi za awali za Mei Mosi
wanagundua mambo mengi ya kipagani yanayohusiana na chanzo cha sikukuu
hiyo.
Watu waliohama Ulaya walipeleka
desturi za Mei Mosi walikoenda, na baadhi ya wazao wao bado husherehekea
sikukuu ya Mei Mosi kidesturi. Hata hivyo, katika nchi nyingi Mei Mosi,
au Jumatatu ya kwanza baada ya tarehe moja Mei, ni sikukuu ya
wafanyakazi.
Mei Mosi Yawa Sikukuu ya Wafanyakazi
Magwaride na maandamano ya
sikukuu ya kisasa ya Mei Mosi yalianzia Amerika Kaskazini. Kwa nini?
Yale mapinduzi ya viwanda yalitokeza mashine zilizofanya kazi mfululizo,
na kwa hiyo wenye viwanda waliwataka wafanyakazi wafanye kazi mfululizo
kwa saa 16 hivi kila siku isipokuwa Jumapili. Ili kuboresha maisha ya
wafanyakazi, vyama vya wafanyabiashara na wafanyakazi huko Marekani na
Kanada vilitaka kuanzia Mei 1, 1886 siku ya kazi iwe na urefu wa saa
nane. Waajiri wengi walikataa ombi hilo, kwa hiyo maelfu ya wafanyakazi
waligoma Mei tarehe 1.
Kwa mara ya kwanza kabisa
wanaharakati wa wafanyakazi waliuawa katika Ghasia za Haymarket huko
Chicago, Illinois, Marekani, na wafanyakazi wengine nchini Hispania,
Italia, Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, na Urusi, waliunga mkono harakati
hizo.*
Mnamo mwaka wa 1889, mkutano wa vyama vya Kisoshalisti ulimwenguni huko
Paris ulitangaza kwamba Mei 1, 1890, ingekuwa siku ya kimataifa ya
maandamano ya kutetea siku ya kazi ya saa nane. Kuanzia wakati huo,
Mei 1 ikawa sikukuu ya kila mwaka ya kutetea masilahi ya wafanyakazi.
Katika jamhuri za Muungano wa
Sovieti, kwa kawaida Mei Mosi ilisherehekewa kwa magwaride ya kijeshi na
maonyesho ya maendeleo ya kiteknolojia. Nchi nyingi leo husherehekea
Siku ya Wafanyakazi tarehe moja Mei. Hata hivyo, Marekani na Kanada
husherehekea siku hiyo Jumatatu ya kwanza ya Septemba.
Uhusiano Kati ya Sikukuu ya Kale na ya Leo
Sikuzote Mei Mosi imekuwa
sikukuu ya umma. Wafanyakazi hawakwenda kazini iwe waajiri wao
walikubali au la. Majukumu yalibadilika. Watu wa kawaida walimwigiza
mfalme na malkia, na mara nyingi watawala walidhihakiwa kwa utani. Kwa
hiyo, Mei Mosi ilikuja kuhusianishwa na harakati za wafanyakazi, na
kufikia karne ya 20, ilitambuliwa na chama cha Kisoshalisti kuwa
sikukuu.
Kama sikukuu ya kale ya Mei
Mosi, Siku ya Wafanyakazi Duniani imekuwa siku ya magwaride mitaani.
Hata hivyo, katika miaka ya karibuni kumekuwa na jeuri katika sherehe za
Mei Mosi. Kwa mfano, mnamo Mei Mosi mwaka wa 2000, kulikuwa na
maandamano ulimwenguni pote ya kupinga ubepari. Waandamanaji walipigana,
walijeruhiwa na kuharibu mali.
Kuleta Mabadiliko Yanayohitajiwa
Je, kweli tunaweza kutazamia
wanadamu walete mabadiliko yanayohitajiwa ulimwenguni pote kwa faida ya
watu wote wanyoofu? Hawawezi. Methali moja ya kale ya Biblia
imethibitika kuwa kweli: “Njia ya mtu wa udongo haimo katika uwezo wake.
Mwanadamu anayetembea hana uwezo wa kuongoza hatua yake.”—Yeremia 10:23.
Nguvu zinazozidi za wanadamu
zinahitajiwa ili kuleta amani ulimwenguni. Chanzo cha nguvu hizo ni
Yehova Mungu, Muumba wa dunia. Neno lake Biblia, linasema kwamba
‘anaufumbua mkono wake na kutosheleza tamaa ya kila kitu kilicho hai.’ (Zaburi 145:16) Tunakutia moyo uchunguze zaidi ahadi za ajabu za Mungu.
Ili kutimiza sala ya kielelezo ambayo Mwana wa Mungu, Yesu Kristo, aliwafundisha wafuasi wake, Ufalme wa Mungu utakuja
na bila shaka mapenzi ya Mungu yatatendeka duniani. Biblia inaahidi
kwamba Yesu Kristo, Mtawala aliyewekwa rasmi na Mungu, “atamkomboa
maskini anayelilia msaada, pia mwenye kuteseka na yeyote ambaye hana
msaidizi. Atamsikitikia mtu wa hali ya chini na maskini, naye ataziokoa
nafsi za maskini. Ataikomboa nafsi yao kutoka katika ukandamizaji na
katika jeuri, nayo damu yao itakuwa na thamani machoni pake.”—Zaburi 72:12-14.
[Maelezo ya Chini]
Kabla ya kalenda
ya Gregory kuanza kutumiwa miaka 400 hivi iliyopita, mwezi wa Mei
ulianza siku 11 baadaye kinyume na ilivyo leo, wakati ambapo kulikuwa na
joto na mimea mingi zaidi.
Ghasia hizo
zilizuka siku moja baada ya wafanyakazi kadhaa kufa katika mapambano
kati ya waandamanaji na polisi wa kutuliza ghasia.
[Picha katika ukurasa wa 12]
Nguzo ya karne ya 16 ya sikukuu ya Mei iliyosimamishwa kila Mei Mosi nje ya kanisa huko London
[Hisani]
From the book Observations on Popular Antiquities
[Picha katika ukurasa wa 14]
Maandamano ya kupinga ubepari, Mei Mosi mwaka wa 2000, London, Uingereza
[Hisani]
© Philip Wolmuth/Panos Pictures