BAJETI 2014/2015 : Prof. Lipumba alia na nakisi ya bajeti
http://jaridahuru.blogspot.com/2014/04/bajeti-20142015-prof-lipumba-alia-na.html
Profesa Lipumba |
Bajeti 2014/2015: Bajeti inayotarajiwa kuwasilishwa hivi karibuni bungeni Dodoma haitakuwa na manufaa yoyote kwa Watazania, iwapo Serikali haitakuwa tayari kupunguza nakisi inayotokana na matumizi makubwa yasiyokuwa ya lazima.
Akizungumza baada ya uzinduzi wa Ripoti ya Ukuaji
wa Kiuchumi kwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara iliyotolewa
na Repoa, Mtaalamu wa Uchumi, Profesa Ibrahim Lipumba alisema tatizo
lililopo kwa sasa ni matumizi makubwa ya Serikali kwa mambo yasiyo ya
lazima, huku ikiwa na mapato madogo.
Profesa Lipumba ametoa maoni hayo siku moja baada
ya Waziri wa Fedha, Saada Nkuya kuliambia gazeti hili kuwa masharti ya
wahisani na utegemezi wa fedha ni mambo ambayo kwa kiasi kikubwa
yanakwamisha utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo nchini.
Pamoja na kukiri imekuwa vigumu kwa Tanzania
kuridhia masharti mapya ya wahisani, pia alikiri kwamba matumizi ya
Serikali yamekuwa makubwa kuliko mapato, hivyo kusababisha nakisi kubwa
katika bajeti ya mwaka 2013/14.
Hata hivyo, Profesa Lipumba alifafanua chanzo cha
tatizo hilo wakati wa uwasilishaji ripoti iliyoandaliwa na Taasisi ya
Utafiti na Kupunguza Umaskini (Repoa) kwa kushirikiana na Shirika la
Fedha Duniani (IMF) ikilenga kuangalia ukuaji wa kiuchumi kwa nchi za
Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwa miongoni.
Alieleza kwamba matumizi hayo ni pamoja na ya
zaidi ya Sh60 bilioni zilizotumika kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba
ambayo hata baada ya kukamilisha kazi yake, Serikali imesimamia
kutotumia mapendekezo ya Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa, hivyo kupoteza
mabilioni ya shilingi za walipa kodi bila sababu.
“Pamoja na matumizi makubwa ya Tume, matumizi ya
Bunge la Katiba bado thamani halisi ya fedha za walipa kodi haiwezi
kulipwa kwa utaratibu ambao Serikali imeamua kuutumia. Hapa tunaona
namna Serikali inavyokuwa na matumizi makubwa ambayo hayana tija kwa
wananchi,” alisema.
Alisema ili kuondoa kasi ya ukuaji wa nakisi,
Serikali pia inatakiwa kufuta kabisa misamaha holela ya kodi inayofikia
Sh1 trilioni na bilioni 800 ambayo ni sawa na asilimia tano ya pato la
taifa.
Alisema miongoni mwa maeneo mengine
yanayosababisha tatizo hilo ni katika miradi inayosimamiwa na Serikali
ambayo mingi imekuwa ya gharama kubwa kuliko uhalisia na gharama
huongezwa kwa kati ya asilimia 30 hadi 50 zaidi ya gharama halisi.
Hata hivyo, akizungumzia ripoti hiyo ya Repoa
iliyoangazia zaidi ukuaji wa kiuchumi kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la
Sahara, alisema japokuwa uchumi huo unakua, haujaweza kuwasaidia
wananchi wa kawaida katika nchi za Afrika.
Awali, mwakilishi wa Shirika la Fedha Duniani
(IMF) nchini, Thomas Baunsgaard alisema japokuwa ukuaji wa uchumi
umekuwa ukitia moyo na Tanzania inafikia asilimia 7.2, bado upunguzaji
wa umaskini unakwenda kwa kasi sana.
Alisema kupungua uzalishaji kwenye sekta ya kilimo
kumechangia ukuaji wa sekta ya utoaji huduma na Dar es Salaam idadi ya
maskini imepungua.