jaridahuru

Mitandao

TANZIA : MCH. MTIKILA AFARIKI KWA AJALI YA GARI: JINSI ILIVYOTOKEA, R.I.P MTIKILA



Pwani/Dar.  Aliyekuwa Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila (65) amefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea katika Kijiji cha Msolwa, Chalinze wilayani Bagamoyo.

Mtikila alifariki dunia jana saa 11.45 alfajiri akitokea mkoani Njombe kurejea Dar es Salaam kwa shughuli za kampeni baada ya gari aina ya Toyota Corrolla alilokuwa akisafiria pamoja na wenzake watatu kuacha njia na kupinduka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jafari Mohamed alisema ajali hiyo ilichangiwa na mwendokasi wa gari hilo.
Alisema Mchungaji Mtikila alikuwa amekaa kiti cha mbele bila kufunga mkanda na hivyo kusababisha arushwe nje ya kupitia kioo cha mbele na gari kumlalia kifuani na kupoteza maisha papo hapo huku abiria wengine wawili na dereva wakijeruhiwa.
Mwili wa marehemu na majeruhi walipelekwa Hospitali ya Tumbi. Wengine waliojeruhiwa ni Mchungaji Patrick Mgaya (57) na Ally Mohamed (42) wote wakazi wa Dar es Salaam na dereva wa gari hilo, George Steven (31) mkazi wa Mbezi Beach aliyekuwa amekodiwa na Mchungaji Mtikila.
Majeruhi asimulia
Akisimulia ajali hiyo, Mchungaji Mgaya ambaye ni nduguye Mtikila alisema walikuwa wakitokea Njombe ambako walifanya mkutano wa kampeni za ubunge na madiwani Jumamosi.
Alisema dereva wa gari hilo alikuwa akiendesha mwendo mkali na licha ya kumsihi mara kadhaa, hakusikia.
Alisema walipofika Msolwa, walipokuta lori limeegeshwa mbele yao upande wa kulia: “Tulipofika maeneo hayo kuna gari ambalo tulikuwa tumeongozana nalo, likatupita kwa kasi na baada ya dereva wetu kutaka kupita, kukawa na lori jingine linakuja, akaamua kulikwepa na kwenda pembeni mwa barabara,” alisema.
Alieleza kuwa baada ya gari lao kwenda pembeni, lilikuta shimo lililosababisha kupinduka mara tatu, ndipo Mtikila alipotoka kupitia kioo cha mbele na gari likamlalia upande wa kushoto kifuani.
“Mwili wake haukuwa na majeraha mbali na kutokwa na damu kidogo mdomoni tu na baada ya hapo tulimtoa na muda mfupi polisi walifika na kuchukua mwili wake,” alisema Mchungaji Mgaya.
Alisema Mchungaji Mtikila alikuwa anataka wawahi kwa sababu alikuwa na mpango wa kusafiri tena kwa ndege jana kwenda Musoma kuendelea na kampeni.
Eneo la ajali
Ajali ilitokea katika eneo la wazi lenye mteremko mkali na lisilokuwa la makazi ya watu. Kutokana na alama za gari hilo tangu lilipohama barabarani na kuingia bondeni, inaonekana lilitembea umbali wa mita 100 na kasha kuruka juu na kugonga mti kabla ya kupinduka.
Kamanda Mohamed alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mbali na mwendo kasi, kuna uwezekano mkubwa pia dereva ambaye anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi, alizidiwa na usingizi.
Rambirambi
Chama cha ACT- Wazalendo kimetuma salamu za rambirambi kikieleza kupokea kwa masikitiko kifo cha ghafla cha Mchungaji Mtikila.
Katika taarifa yake, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Samson Mwigamba alitoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu jamaa na marafiki na Watanzania kwa msiba huyo.
“ACT wazalendo inatambua mchango wa kina wa kutafuta mageuzi ya kweli yaliyokuwa yakiendeshwa na Mchungaji Mtikila wakati wa uhai wake. Tunaamini mchango wake kwa Taifa ulikuwa unahitajika kwa kiasi kikubwa hasa wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu,” alisema Mwigamba.
Source Mwanachi;
Credits : Julieth Ngarabali, Sanjito Msafiri, Kelvin matandiko na Bakari Kiango

Related

Siasa 5351613531568260824

Post a Comment

emo-but-icon

Wadhamini

UJUMBE

JH Katika Facebook

Nyayo zetu twitter

Za Juu

Mitandao

Piga Kura

Je ungependa Tanzania iwe na serikali ngapi?
  
pollcode.com free polls 

ADVERTISEMENTS

Msimamo wa ligi mbalimbali

Football results provided by whatsthescore.com

Mechi Live

Walioko Hewani Kwa Sasa

item