SOKA: MBEYA CITY YAMGEUZIA KIBAO JOHN BOCCO
http://jaridahuru.blogspot.com/2015/10/soka-mbeya-city-yamgeuzia-kibao-john.html
Dar es Salaam. Klabu ya Mbeya City imewasilisha taarifa ya rufaa kwenda Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ikieleza upungufu mwingi na kutaka wachezaji wa Azam wachukuliwe hatua za kinidhamu.
Katibu mkuu wa klabu hiyo, Emmanuel Kimbe aliwataja John Bocco na Mudathir Yahya kuwa inafaa wachukuliwe hatua za kinidhamu. Pia, Mbeya City inadai Bodi ya Ligi (TPLB) ilikosea kimsingi kumwadhibu Nyoso na kuwaacha wawili hao.
Aidha, klabu hiyo inadai TPLB ilikosea kufikia uamuzi huo wa usala hilo kwa kikao kilichoongozwa na mwenyekiti wa Azam, Said Mohammed, huku klabu yake ikiwa mlalamikaji.Kimbe alieleza kuwa kifungu namba 37 (24) cha kanuni za ligi kilichotumika kumwadhibu Nyoso na kumfungia miaka miwili na faini ya Sh2milioni, kilitumika vibaya.
Aidha, klabu hiyo ilieleza kuwa baadhi ya wachezaji wa Azam waliwashambulia wachezaji wao, akiwamo Christian Sembuli aliyepigwa kibao mbele ya mwamuzi.
“Klabu yetu inapenda umma wa wanamichezo nchini ujue kuwa inasononeka na matukio yoyote yenye kuupunguzia ladha mchezo wa soka kunakofanywa na yeyote.
“Mara zote klabu yetu imekuwa ikisisitiza na kusimamia nidhamu ya wachezaji na viongozi muda wote wanapotekeleza majukumu yao,” ilieleza klabu hiyo.
Alisema baada ya tukio hilo, iliunda kikosi kazi kuliangalia suala zima na kilipewa saa 86 na kilifanyia kazi hadidu rejea kadhaa, ambazo ni pamoja na kupitia rejea za mchezo huo.
Alisema wanapata shaka kuhusu uamuzi ya kamati husika kutokana na kikao kilichotoa uamuzi kuongozwa na mwenyekiti wa kamati hiyo, Said Mohamed.
Taarifa hiyo ilisema kamati ya usimamizi na uendeshaji ya TPLB pamoja na mambo mengine inashughulikia kufanya uamuzi kwa masuala yote, ambayo uamuzi wake haukatiwi rufaa kama yalivyoainishwa katika kanuni namba 74 ya Ligi Kuu. Kanuni iliyotumika kutoa adhabu, namba 37(24), si miongoni mwa zile ambazo hazikatiwi rufaa, ni kanuni inayopaswa kutumiwa na kamati ya maadili au nidhamu, ambayo kulingana na aina ya kosa linahitaji kuthibitishwa pasipo shaka na pande zote zinazohusika.
Alisema hata kama kanuni waliyoitumia ingekuwa ni sahihi, tafsiri ya kanuni, hasa maneno au na hayakutumika ipasavyo kwa kuwa walikuwa na uchaguzi wa adhabu, lakini adhabu hizo haziendi pamoja kama kamati ilivyotafsiri.
“Adhabu imeangalia upande mmoja wa hisia , hivyo kutoa adhabu kubwa bila kuangalia upande wa mchezaji husika.
“Pia, kamati imeunganisha adhabu zote kwa pamoja wakati kanuni inatoa nafasi ya adhabu moja kwa wakati mmoja,” alisema Kimbe.
Kanuni ya 37(24) inasema, “mchezaji atakayepatikana na hatia ya kufanya makosa makubwa ya kimaadili au kinidhamu, au ya kibaguzi au ya kidhalilishaji au yatakayotafsiriwa kuwa ni ukiukaji mkubwa wa taratibu za mchezo na ubinadamu atatozwa faini kati ya Sh1 milioni mpaka tatu au/na kusimamishwa kushiriki michezo mitatu mpaka kumi ya klabu yake atakayoitumikia katika ligi na mashindano mengine rasmi ya TFF au kufungiwa kipindi cha kati ya mwaka mmoja na miwili.”
“Pia, mchezaji anayetuhumiwa (Nyoso) hakupewa nafasi ya kusikilizwa na kamati kama misingi ya utendaji haki inavyohitaji kwa mujibu wa kanuni ya 37(24), klabu inaona mchakato mzima wa usikilizaji wa shauri hili umeingia dosari, hivyo uamuzi na adhabu iliyotolewa inakosa sifa kisheria,”alisema Kimbe.
Klabu hiyo imedai kutilia shaka ushahidi uliotumika na kutafsiriwa na kamati kufanya uamuzi kwani kuna uwezekano iliangalia picha mnato iliyosambaa kwenye mtandao baada ya mchezo huo na kuzua mjadala katika jamii, bila kuangalia mazingira mengine ya tukio hilo.
Katibu mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa alipoulizwa jana alisema bado rufaa ya Mbeya City hajaipata, ingawa anasikia walikuwa na mpango wa kutuma na endapo wakiipata watawasilisha kunahusika kwa hatua zitakazofuata.