jaridahuru

Mitandao

ELIMU: ZIFAHAMU MBINU ZA WATOTO KUJISOMEA ILI UMJENGEE MWANAO UWEZO WA KUJISOMEA



Wazazi wengi wanaamini kuwa elimu ndiyo mkombozi mkubwa wa maisha ya watoto wao.
Kila mzazi ana ndoto ya kuona mtoto wake akiwa na maisha bora, na kwa walio wengi maisha bora hayana njia ya mkato zaidi ya mtoto kujipinda kusoma.
Wazazi wanaojua umuhimu huu utawaona wakijihimu kuhakikisha watoto wao wanajifunza kama anavyobainisha mzazi, Salumu Kesi:
‘’Kwa nchi kama Tanzania ambayo sioni future nzuri (mustakabali mzuri) kwa wananchi wake, ni mzazi mzembe na pengine punguani atakayeshindwa kujenga mazingira bora ya elimu kwa kizazi chake.’’
Kesi ambaye ni mzazi wa mtoto mmoja wa miaka sita anasema kwa kuwa alishatambua umuhimu wa elimu mtoto wake, alianza kumjengea mazingira ya kujifunza na kujali elimu tangu akiwa na mwaka mmoja.
‘’ Naweza kukuonyesha hata picha nilipokuwa nikimpakata nilikuwa nina kitabu au gazeti pembeni. Nilitaka macho yake yazoee vitabu. Alipoanza kuzungumza na kutambua vitu kama picha nilimwonyesha picha za magazetini na vitabuni... kuna wakati aliniomba vitabu na kuanza kusoma kwa lugha anayoijua yeye na nilimrekodi, unaweza kucheka namna alivyokuwa akisoma,’’ anaeleza.
Bila shaka Kesi anaakisi ukweli uliomo katika msemo wa Kabila la Ibo la nchini Nigeria unaosema: Ng’ombe jike anapokula, watoto wake humwangalia.
Miaka michache baadaye mtoto wa Kesi akiwa na miaka sita tu maishani, ameshaanza kuwa na mapenzi makubwa ya kujisomea. Ni sawa na ndama aliyekuwa akimwangalia mama yake akila. Alimuona baba akisoma, sasa ni zamu yake kuiga.
Je, wazazi wa Kitanzania tunauishi msemo huu? Kama tunavyohangaikia mkate wa kila siku, ndivyo tunavyoshughulika na kuwaandaa watoto kujua umuhimu na thamani ya kujifunza na kupenda elimu?
Mtunzi na mdau wa vitabu, Deo Simba anasema kuwa ili kukuza mapenzi kwa vitabu na usomaji ni muhimu kuanza na watoto kwa kuwapa vitabu vya kusoma.
‘’ Jamii nzima tuna nafasi katika kukuza utamaduni huu. Badala ya kuwanunulia watoto pipi zinazoishia kuleta migogoro ya kiafya, hasa afya ya kinywa, basi tuwanunulie vitabu, walau kimoja kila mwezi,’’ anaeleza.
Mbinu za usomaji
Ili tusiwe wazembe na pengine punguani kama anavyosema Kesi, makala haya yanaangazia mbinu kadhaa anazoweza kutumia mzazi kuwa na utamaduni wa kujisomea na kujifunza kwa jumla.
Mwalimu Joyce Kirabo anasema mbinu ya kwanza ya kujenga mtazamo chanya wa mtoto kuhusu kujifunza na kupenda elimu ni mzazi kumtambulisha katika anachokiita ‘shughuli za kitaaluma’
Ni shughuli zipi hizo? Anataja kuwa ni pamoja na kusoma vitabu, kuchora, kumfanyisha hesabu nyepesi, kumfundisha sarufi za msingi na misamiati mipya
“ Mnunulie vitu vya kujifunzia na ukimpa kitabu usiondoke, soma naye. Watoto wanapenda kuangaliwa na wazazi wanapofanya kazi. Anapoanza kujifunza mwenyewe na kujitegemea, unaweza ukapunguza muda wa kuwa naye anapojifunza, ‘’ anafafanua.
Anza wewe kujifunza. Kirabo anasema moja ya misingi mizuri ya mafanikio ya kujifunza kwa mtoto ni pale anapojifunza kutoka kwa wazazi wake. Kiigizo cha kwanza cha mtoto kupenda kusoma na kujifunza hakina budi kuwa wazazi kama walimu wa kwanza wa mtoto.
“ Anza wewe kujisomea ili mtoto wako akuone, akiiga na akawa na uzembe fulani, usikasirike mpe muda kwa kuwa baadhi ya watoto wanahitaji muda kubadilika,’’ anaeleza.
Tenga muda wa kuzungumza na mtoto wako kuhusu elimu. Mbinu hii inawashinda wazazi wengi na aghalabu hoja wanayoitoa ni kuwa hawana muda kwa kuwa wanatingwa na mihangaiko ya dunia.
Hata hivyo, Kesi anasema hoja hiyo haina mashiko na mara nyingi anasema inatolewa na wazazi anaowaita wazembe.
‘’ Ni haki ya mzazi kutafuta maisha kwa ajili ya familia, lakini pia ni haki nyingine kwa mzazi huyohuyo kuwa na muda wa kuzungumza na familia yake. Ni udhaifu mkubwa kwa mzazi
kushindwa kutafuta japo dakika tano kwa mwezi kuzungumza na mtoto masuala ya shule,’’ anaeleza.
Tunawapa watoto wetu zawadi gani? Kisaikolojia hujenga ukaribu na watoto wa kupitia zawadi, lakini tumejiuliza aina bora ya zawadi tunazopaswa kuwapa watoto wetu? Je tuendelee kuwapa watoto wetu midori, vitu vya kuchezea, pipi na zawadi nyingine za aina hiyo?
Ni wakati wa kubadilika, wazazi hatuna budi kutumia zawadi kama mbinu ya kuwajenga watoto kuwa na tabia ya kujifunza. Tuwanunulie zawadi zenye mrengo wa kuimarisha ubongo badala ya kuviza uwezo wa akili zao tangu mapema.
Moja ya zawadi hizi ni vitabu. Mwanaharakati maarufu wa mazingira Afrika na mshindi wa nishani ya amani ya Nobel, Profesa Wangari Maathai anaifananisha tabia ya usomaji vitabu na anachokiita ‘kilimo cha akili’’.
Mbinu nyingine ni kuwa na ukaribu na walimu. Unaweza usimuulize mtoto maendeleo yake darasani, lakini ukapata picha kamili ya maendeleo yake kutoka kwa walimu.
Hata hivyo, mbinu hii bado inawashinda wazazi wengi. Siyo tu hawana muda wa kwenda shule na kuzungumza na walimu, wanashindwa kutumia mbinu nyingine za mawasiliano kama simu za mkononi.
Mzazi, Bakari Heri hahisi tabu kwenda shule kuulizia maendeleo ya mwanawe anayesoma chekechea. Anasema asipokwenda atapiga simu kwa mwalimu au mmiliki wa shule.
‘’ Huyu wangu anasoma vidudu (elimu ya chekechea), lakini tazama namna ninavyohangaikia maendeleo yake. Hali itakuaje akifika sekondari? Lakini kwa nini nafanya haya yote? Najua thamani ya elimu, natambua kuwa ubora wa nyumba huanza katika msingi,’’ anasema.
Wakati Heri anawasumbua walimu kuhusu maendeleo ya mtoto wake, uzoefu unaonyesha wazazi wengi si tu hawana mawasiliano ya karibu na walimu, lakini wanashindwa kuhudhuria vikao vya wazazi.
Ni kwa sababu hii si ajabu kuona mkutano katika shule yenye watoto zaidi ya 500 ukihudhuriwa na wazazi chini ya 50.
Wazazi wengi ama hawajui wajibu wao au wanatoa hoja ya kutingwa na shughuli za kimaisha, ambayo hata hivyo inapingwa na mdau wa elimu, Joseph Ambali anayesema:
‘’Kutafuta maisha ni hoja mfu, hao wanaotafuta maisha wanafanya hivyo kwa ajili ya haohao watoto. Kwa nini elimu yao isiwe sehemu ya maisha wanayotafuta? Huwezi kushindwa kwenda shule kwa miaka saba anayosoma mtoto kwa kisingizo kuwa siku zote umetingwa na maisha.’’
Bila shaka Kesi na Heri ni wazazi wanaojitambua; ni wazazi wanaojua wajibu wao kwa viumbe waliochangia kuwaleta duniani. Wazazi wengi wa Kitanzania wanajua kuzaa, malezi wanaichia dunia. Huenda wazazi hawa wakawa ni wale ambao Kesi anawaita kuwa ni mapunguani, je, wewe ni mmoja wao?

SOURCE:
MWANANCHI

Related

Habari Mpya 6321369025274140918

Post a Comment

emo-but-icon

Wadhamini

UJUMBE

JH Katika Facebook

Nyayo zetu twitter

Za Juu

Mitandao

Piga Kura

Je ungependa Tanzania iwe na serikali ngapi?
  
pollcode.com free polls 

ADVERTISEMENTS

Msimamo wa ligi mbalimbali

Football results provided by whatsthescore.com

Mechi Live

Walioko Hewani Kwa Sasa

item