BUNGENI: UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA KITENDAWILI IWAPO UKAWA HAWATARUDI BUNGENI, WAOMBWA KUACHA HASIRA
http://jaridahuru.blogspot.com/2014/07/bungeni-uchaguzi-serikali-za-mitaa.html
Tanga. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema hatima ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu utategemea uamuzi wa wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kurejea katika Bunge Maalumu kuipitisha Katiba Mpya kwa wakati.
Pinda alisema hayo jana katika kikao chake na
mameya na wenyeviti wa halmashauri za wilaya na miji nchini uliofanyika
hapa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Serikali za Mitaa.
“Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu
umegubikwa na kitendawili kutokana na wajumbe wa Bunge hilo kugawanyika
na kushindwa kufanya kazi waliyopewa kwa wakati ili Katiba iweze
kupatikana mapema.
“Ni kama kitendawili kidogo kwa sababu bado Bunge
la Katiba wanavutana. Tuna changamoto hiyo, tunaendelea kumwomba Mungu
ili Ukawa waondoe hasira warejee bungeni,” alisema Pinda.
Hata hivyo, alisema ofisi yake inajiweka tayari
kwa uchaguzi huo mwaka huu kama ulivyopangwa na kwamba hata kama
utasogezwa, mipango iwe imeandaliwa na kuwa tayari kwa wakati wowote.
Alisema hata kama itatokea vinginevyo, Serikali
kwa upande wake haikatazwi kuendelea kufanya maandalizi, ndiyo maana
ofisi yake iko kwenye pilikapilika za kuweka mambo tayari kwa ajili ya
kufanikisha uchaguzi huo.
“Sisi tunakwenda na yote mawili, kama utakuwapo
mwaka huu na hata kama utasogezwa mbele kwa sababu tusipofanya
maandalizi nyie wenyewe mtakuja kunigeuka,” alisema Pinda.
Kauli hiyo ya Pinda imekuja wakati viongozi wa
Ukawa wakisisitiza kuwa hawatarudi bungeni hadi pale
watakapothibitishiwa kuwa Rasimu ya Katiba itakayojadiliwa ni ile
iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Wajumbe wa Ukawa ambao ni wajumbe wa bunge hilo
kutoka vyama vya CUF, NCCR-Mageuzi, Chadema na baadhi kutoka Kundi la
201, walisusia bunge hilo wakidai kuwa wenzao wa CCM walikuwa wanataka
kuingiza rasimu mpya inayoendana na mfumo wa Serikali mbili badala ya
rasimu ya Tume iliyopendekeza serikali tatu.
Maandalizi ya uchaguzi
Waziri Mkuu alisema maandalizi ya uchaguzi huo
yanakwenda vizuri na kwamba hatua inayoendelea sasa ni uchambuzi wa
maombi yaliyowasilishwa Tamisemi ya kuongezwa mitaa, vitongoji, vijiji
na kata. Alisema hatua ya uchambuzi wa maombi ya vijiji, vitongoji,
mitaa na kata mpya yapo mwishoni kabla ya kupitishwa rasmi na kupelekwa
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hatimaye kuingizwa kwenye orodha ya
uchaguzi.
Pinda aliwataka mameya na wenyeviti wa halmashauri
nchini kuhakikisha wanasimamia ipasavyo jukumu la ukusanyaji wa mapato
ya ndani ya Serikali Kuu ili kuwezesha Taifa kuwa na fedha za
kujiendesha.
“Katika hili sitakuwa na huruma kwa sababu bajeti ya safari hii
tulishuka sana, halmashauri mlilala badala ya kutimiza wajibu wenu wa
kukusanya mapato ipasavyo,” alisema Pinda.
Aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini
kuhakikisha wanampelekea taarifa za kila miezi mitatu za kuelezea namna
zilivyokusanya mapato na zionyeshe kuwa imefikiwa asilimia 100.