SIASA: VIONGOZI WANAO WABEZA WABUNGE KUTAJWA BUNGENI
http://jaridahuru.blogspot.com/2014/05/siasa-viongozi-wanao-wabeza-wabunge.html
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amemtaka Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kusini Deosderius Mipata (CCM) kuwataja viongozi wa Serikali wanaobeza wabunge katika suala zima la utekelezaji wa maendeleo katika maeneo yao.
Alitoa kauli hiyo bungeni jana baada ya Mbunge huyo kudai kuwa baadhi ya viongozi Serikali wamekuwa wakibeza juhudi za wabunge ambao kimsingi walichaguliwa na wananchi.
“Pamoja na juhudi na ukweli ulizoeleza wapo watendaj na viongozi wa Serikali wanaobeza juhudi za wabunge kwani kwa miaka mitatu tangu niwe Mbunge nimekuwa nikihangaika sana na nimepata kiasi kidogo tu cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara , Serikali ina kauli gani juu ya watendaji wanaobeza juhudi za viongozi waliochaguliwa na wananchi?”
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu alimtaka Mbunge huyo kufanya kazi yake akiwa kama kiongozi wa wananchi.
“Wewe ni Mbunge jukumu lako unalifahamu hata kama watu watasema wewe tekeleza wajibu wako ukipata nafasi ninong’oneze kidogo ili nipate kuwafahamu,” alisema Waziri Mkuu.
Akijibu swali la Msingi Waziri Mkuu alisema dhamira ya Serikali ni kuona kuwa ahadi zote zinatekelezwa.
Alisema kiasi cha Sh bilioni tatu kiliombwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara lakini walipata milioni 800 jambo linaloonesha Serikali ina dhamira ya ujenzi wa barabara hiyo.
Alisema cha muhimu ni kuangalia bajeti ya sasa itasaidiaje katika kumaliza suala hilo. Katika swali la msingi, Mbunge huyo aliuliza dhamira ya Serikali kumaliza ujenzi wa barabara.
“Je Serikali bado inawaaminisha wananchi ahadi zitatekelezwa kabla ya kipindi kuisha kwani mwaka 2010 wakati wa kampeni za uchaguzi Rais Jakaya Kikwete alitoa ahadi kwa wananchi wa jimbo hilo na ilichukuliwa kama mkataba wake baada ya kuchaguliwa.
Chanzo:Habarileo