AFYA: ETI KUPIMA 'DENGUE' 50,000? HII NDIO BONGO BWANA!
http://jaridahuru.blogspot.com/2014/05/afya-eti-kupima-dengue-50000-hii-ndio.html
Dar/Dodoma. Wakati taharuki iliyosababishwa na
mlipuko wa homa ya dengue ikiendelea kutikisa kila kona ya jiji,
imebainika kwamba gharama za vipimo katika hospitali mbalimbali
zinafikia Sh50,000, ikiwa ni tofauti kubwa na Sh1,000 kwa kipimo cha
malaria.
Ugonjwa huo unazidi kusambaa jijini Dar es salaam
na baadhi ya mikoa, kiasi cha mamlaka kuagiza mabasi yote yaendayo
mikoani yafanyiwe usafi wa kunyunyizia dawa za kuua wadudu kudhibiti
usienee zaidi mikoani. Pia wananchi wameshauriwa kuvaa nguo ndefu ili
kudhibiti mbu wanaoeneza ugonjwa huo mchana tofauti na mbu wa malaria.
Timu ya waandishi wa Mwananchi ilipita katika
baadhi ya hospitali kubwa binafsi na za Serikali jijini Dar es Salaam na
kubaini kuwa gharama ya kupima homa hiyo ni kubwa zaidi katika
hospitali na vituo binafsi vya afya, lakini wagonjwa wanaokwenda katika
hospitali za Serikali hulazimika kulipa kati ya Sh25,000 na Sh30,000.
Pamoja na homa hiyo kufananishwa na malaria kwa dalili na kuenezwa na
mbu, gharama za vipimo vyake ni tofauti kwani mgonjwa wa malaria hutozwa
kati ya Sh1,000 na 2,000.
Hata hivyo, jambo la kutia moyo ni kwamba baada ya
mgonjwa kupata majibu na kubainika anaumwa homa ya dengue, gharama za
tiba huwa ndogo kati ya Sh200 na 500 za kununulia dozi ya dawa za
kutuliza maumivu aina ya panadol.
Wanaopima waongezeka
Mchunguzi wa magonjwa katika maabara ya kimataifa
ya Lancet, Kanda ya Tanzania, Mohamed Abdulai alisema idadi kubwa ya
watu wanakwenda katika maabara hiyo kupima homa ya dengue tangu ugojwa
huo uenee kwa kasi kati ya Machi na Aprili mwaka huu.
Alisema kwa siku wagonjwa zaidi ya 40 hupima
dengue na katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja, wagonjwa 53
waligundulika kuwa na homa hiyo.
Abdulai alisema gharama za kipimo cha dengue katika kituo hicho ni Sh50,000.
Katika Hospitali ya Aga Khan, Mkurugenzi wa Tiba,
Dk Jaffer Dharsee alisema kipimo cha homa ya dengue ni kati ya Sh35,000
hadi Sh40,000 kutokana na mchakato wa upimaji wake.
“Ni lazima tunapompima mtu dengue pia tumpime na
maradhi mengine kwanza kama homa ya matumbo, malaria na maradhi mengine
ambayo tunahisi anayo na ndiyo gharama inakuwa kubwa,” alisema Dk
Dharsee.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Hindu Mandal, Dk
Kaushik Ramaiya alisema katika hospitali hiyo kipimo cha homa ya dengue
ni Sh30,000. “Tunatumia vipimo vitatu, kile kitakachoangalia iwapo
chembe hai nyeupe za damu zimepungua, malaria na kiwango cha sumu
kinachotokana na virusi vya dengue,” alisema.
Dk Ramaiya alisema tangu vyombo vya habari vianze
kuripoti ugonjwa huu, watu wamejawa hofu na hufika hospitali kwa wingi
wakitaka kupima maradhi hayo ili kujua kama wapo salama.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Meshack Shimwela alisema
baada ya vipimo vilivyotoka maabara kuu ya Serikali kumalizika, gharama
ya vipimo hivyo zimefikia Sh25,000.
“Hospitali imetumia fedha zake kununua vipimo 10
ambavyo viligharimu Sh250,000, hata hivyo kwa sasa vimekwisha hivyo
mgonjwa hana budi kuchangia,” alisema. Hata hivyo, alisema inapotokea
mgonjwa mwenye hali mbaya na hana uwezo, humpima bure.
Daktari kiongozi wa Hospitali ya Mwananyamla,
Mrisho Lupinda alisema awali wagonjwa wa dengue walipimwa bure na
taasisi ya Afya ya Ifakara, lakini uongozi wa hospitali yake unatarajia
kununua vipimo kwa Sh480,000 na baada ya kupatikana, uongozi utapanga
gharama za upimaji.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Temeke, Amani
Malima alisema wana uhaba wa vipimo ingawa kwa sasa wanatumia vichache
vilivyopo kusaidia wagonjwa wa dharura.
Katibu CCM augua
Katibu Mwenezi wa CCM wa Wilaya ya Mufindi, Daud
Yassin ameugua ugonjwa wa dengue akiwa jijini Dar es Salaam kwa shughuli
binafsi.Yassin alisema aligundulika kuwa na ugonjwa huo alipokwenda
Hospitali ya Dk Mvungi iliyopo Kinondoni jana ambako alilipia Sh60,000
kwa ajili ya kipimo.
“Wiki iliyopita nilikuwa nasumbuliwa na malaria,
nikatumia dozi nikamaliza, lakini sikuwa na nafuu. Homa iliongezeka na
kichwa kikazidi kuuma, usiku wa kumkia leo (jana) hali ilikuwa mbaya
sana,” alisema. Yassin, ambaye ni mratibu wa mashindano ya Kombe la
Muungano Mufindi, alisema kutokana na kuzidiwa alimpigia simu rafiki
yake mmoja wa Iringa ambaye ni daktari na baada ya kumwelezea dalili
hizo, alimshauri aende hospitali kwa sababu alikuwa na dalili zote za
dengue.
“Nilipokwenda Hospitali ya Dk Mvungi,
nilipumzishwa pale, nikafanyiwa ‘full blood picture’ na kugundulika kuwa
na dengue, ni ugonjwa unaotesa sana,” alisema Yassin.
Serikali yaongeza vipimo
Akitoa taarifa bungeni jana, Naibu Waziri wa Afya
na Ustawi wa Jamii, Dk Stephen Kebwe alisema hadi sasa Serikali imetumia
Sh132 milioni na kutenga Sh500 milioni katika mapambano dhidi ya
ugonjwa huo.
Dk Kebwe alisema wizara yake imejipanga
kuhakikisha vitendanishi vyote vinakuwepo na tayari imeagiza vipimo 750
vya nyongeza, kwa kuwa vipimo vilivyo sasa ambavyo ni 350 vinaweza
kutumika kwa miezi miwili.
Mabasi yapulizwa dawa
Dk Kebwe alisema Serikali imeanza utaratibu wa kupuliza dawa ya
kuua wadudu wakiwamo mbu kwenye mabasi na maeneo yote yenye watu
wanaoingia na kutoka Dar es Salaam, ili kuepuka ugonjwa wa dengue
kusambaa nchini.
Akizungumza muda mfupi baada ya kutoa kauli ya
mawaziri bungeni kuhusu ugonjwa huo, Dk Kebwe alisema hatua hiyo
inafanywa na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi)
kwa kushirikiana na wizara yake.
“Mkoa wa Dar es Salaam, umeanza zoezi la kupulizia
viatilifu vya kuua mbu katika mabasi yanayoingia na kutoka Dar es
Salaam,” alisema Dk Kebwe, kauli ambayo iliungwa mkono na Mkuu wa Mkoa
wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki.
Awali, Dk Kebwe alisema wananchi wanatakiwa kuvaa
nguo ndefu, kutumia vyandarua vyenye dawa na kuweka nyavu kwenye
madirisha na milango ya nyumba ili kujikinga na ugonjwa huo.
Alisema mbu huyo anayeishi katika mazingira ya
binadamu huuma mchana ndani ya nyumba au kwenye maeneo yenye vivuli,
hususan majira ya asubuhi na jioni kabla jua halijazama.
Temeke wamuaga Dk Buberwa
Jana wafanyakazi wa Hospitali ya Temeke waliuaga
mwili wa Dk Gilbert Buberwa aliyefariki dunia Jumapili kutokana na homa
ya dengue.
Sadiki, aliyeongoza wafanyakazi hao, alisema:
“Tumepoteza nguvu kazi muhimu katika sekta ya afya, tena kwenye Kitengo
cha Magonjwa ya Akili. Alikuwa kijana mdogo na alitegemewa sana.”
Mwili wa Dk Buberwa ulihifadhiwa hospitalini hapo
tangu alipofariki katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa
amepelekwa kwa dharura baada ya hali yake kuwa mbaya.
Baada ya wafanyakazi kuuaga mwili huo kwa majonzi
na vilio, ulipelekwa nyumbani kwa marehemu, Tabata Kinyerezi kusubiri
taratibu nyingine za mazishi leo jioni.
Imeandikwa na Florence Majani, Andrew Msechu, Julius Mathias, Beatrice Moses na Sharon Sauwa
Chanzo:Mwananchi